Tuesday, March 22, 2016

JINSI YA KUTOA PEPO WABAYA/CHAFU

Ndugu msomaji,
Maana ya neno pepo linamaanisha, pepo mbaya, shetani, mwovu, mharibifu na mwangamizi. Hao ni malaika waliomuasi Mungu wakatupwa duniani. “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na Yule joka (Shetani), Yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; Nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, Yule mkubwa, Yule wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” Ufunuo 12:7-9.
1. Ili kutoa pepo, kuna mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa:
Ni lazima uwe na nguvu za Roho Mtakatifu.Tunaweza kujifunza kwa Yesu alivyoweza kutoa pepo kwa uwezo na nguvu za Roho. Imeandikwa, “…..awaaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.” Luka 4:36.
2. Kutoa pepo kwa jina la Yesu. Aliye na amri na mamlaka ya kutoa pepo ni mkristo ambaye amemwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake. “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo……” Mathayo 16:17. Wale ambao bado hawajamwamini Yesu na kuokoka, Si vyema kujaribu kutoa Pepo kwa sababu hatatoka, vile vile wanaweza kushambuliwa na hao walio na Pepo, kama wale wana wa Skewa, Kuhani Mkuu.
“.....wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nakuapisha kwa Yesu, Yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, Kuhani Mkuu, walifanya hivyo..... na yule mtu aliye pagawa na pepo wachafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” Matendo 19:13-16.
3. Kufanya maombi kila siku na wakati mwingine kufunga. Bila kufanya hivyo haiwezekani kwa neno lolote, ndio maana Yesu alisema “Lakini kwa namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.” Mathayo 17:21.
4. Kutoa pepo kwa imani. Unaweza kujifunza kwa wale wanafunzi wa Yesu waliposhindwa kumtoa pepo Yule kijana. Walishindwa kwa sababu ya upungufu wa imani. Wangekuwa na imani wangeweza kumtoa Yule pepo. “Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakisema, mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia kwa sababu ya upungufu wa imani yenu…..” Mathayo 17:19-20.
5. Kutoa pepo kwa amri na mamlaka. Unaamuru kwa jina la Yesu atoke naye hutoka. Tunaweza kujifunza kwa Mtume Paulo alivyomtoa pepo Yule kijakazi, akaamuru kwa kumwambia Yule pepo, “..…nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo mtoke huyu, Akamtoka saa ile ile.” Matendo 16:18.
6. Makosa yanayofanyika kwa wale ambao wanakemea pepo, kwa kuwaambia ninakuangamiza kwa damu ya Yesu, ninakuteketeza kwa moto, au ninakufunga. Kufanya hivyo ni kinyume na mamlaka ya Mungu aliyowapa watoto wake. Kwa sababu hiyo, Mungu hajatupa mamlaka ya kuwaangamiza, Kuwateketeza, wala kuwafunga. Bado pepo watakuwepo katika dunia hii kwa sababu wakati wao wakuhukumiwa na kuteswa haujafika. Ndio maana pepo walipomuona Yesu, “…..wakasema,Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” Mathayo 8:23.
7. Wakati wa kumhudumia mwenye pepo si sahihi au lazima kuongea na mapepo na kuwaliza maswali wametoka wapi, nani akawatuma, ni kwa nini wanamtesa huyo mtu, ingawa kuwauliza maswali kunaweza kukupa ufunuo fulani. [Yesu Akamkemea, Akisema, fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka( Marko 1:25-26).] Hatupaswi kumsikiliza shetani na mapepo yake kwa sababu wao ni waovu na waongo siku zote. “....Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewwe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo” Yohana 8:44. Yesu Kristo hakufanya hivyo ambaye ndiye kielelezo chetu katika utumishi, ijapokuwa alimwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na kuteseka siku nyingi alimuuliza swali akitaka kujua jina lake, si jina la pepo.Badala yake pepo waliokuwa wamemtawala yule mtu walijibu wao ni jeshi. “Yesu akamwuliza jina lako nani? Akasema jina langu ni jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia”. Luka 8:30.
Pepo atolewapo hutaka kurudi.
Pepo anapotolewa ndani ya mtu aliyempagawa huondoka na baadae hurudi na kuangalia kama anaweza kuingia tena.Ikiwa mtu huyo anaishi maisha ya dhambi huona nyumba ni chafu na kuingia."Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, aspate. Halafu husema, nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda akachukua pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya". Mathayo 12:43-45.
MAMLAKA YA KUTOA PEPO UMEPEWA NA YESU
Marko 16:17-18 inasema, "ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina Langu watatoa pepo...." Kila Mkristo anao uwezo wa kuwatoa pepo! Sio swala la kwamba "una nguvu" kiasi gani au jinsi gani upo "kiroho" ; cha muhimu ni kuwa Yesu Amekupa mamlaka Yake; unatembea katika jina Lake.
Shetani hana haki ya kuendesha mambo katika maisha yako, au nyumbani mwako au katika maisha ya wale uwapendao. Tumia mamlaka yako katika Kristo dhidi yake.
JE, NI WAKATI GANI UNAWEZA TOA PEPO
Unaweza kuwatoa pepo siku yoyote, muda wowote na mahala popote, kwa kutumia jina la Yesu tu. Usijadiliane naye; mtoe!
Unaweza ukajiuliza. "Nitajuaje kuwa pepo ametoka ninapomkemea?" Hilo ni rahisi. Yesu Alisema, unapowaambia pepo watoke, hutoka. Neno Lake Linakamilisha hilo. Kazi yako ni kumkemea pepo atoke, na jukumu lake pepo ni kutii.
Ingawa, wakati mwingine pepo hujionesha na kulia kwa sauti pindi wanapomtoka yule mtu unayewatoa kwake. Mfano ni kama tulivyosoma katika mstari wetu wa ufunguzi. Pia tunaona tukio kama hilo katika matendo 8:6-8 pale Filipo alipomuhubiri Kristo kwa watu: "...pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu..."
NINI KINAWEZA TOKEA WAKATI WA KUTO PEPO
Hivyo, katika kutoa pepo, roho waovu huweza kupiga yowe na kelele kwa kuteseka pindi wanapotoka; na kisha badiliko la wazi kwa wale ambao pepo wamewatoka hujionesha kuwa kuna tofauti.
Hata hivyo, haijalishi pepo wamepiga yowe au kelele wakati ulipowakemea; cha muhimu ni kile Yesu Alichokisema,"...kwa jina Langu mtatoa pepo..."( Marko 16:17). Huo ndiyo uhalisia, na unapaswa kuwa ndiyo msingi wa imani yako. Hivyo, unapowakemea pepo, wanakuwa hawana chaguo lolote- zaidi ya kukimbia.
Somo Zaidi:
Luka 10:18-19 Akawaambia, Nilimwona shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, Nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na ng'e, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.
Matendo 16:16-18 Ikawa tulipo kuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye juu, wenye kuwahubiria Njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo Akakasirika, akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.
Ndugu msomaji,
Nategemea umesha elewa kuwa, umepewa haki ya kuyatoa MaPepo, na anza kulitoa pepo ambalo linakusumbua, Ndio, unaweza kutoa pepo yako chafu. Biblia inasema kuwa (Marko 16:17-18) = [Ishara hizi zitawafuata Waaminio, watatoa pepo"], umepewa Mamlaka ya kutoa pepo, sio pepo wa mwenzako tu, la hasha, hata pepo ambayo imo ndani yako.
Mamlaka unayo na anza kufanya kazi ya Bwana.
Mungu akubariki sana,
Ni mimi Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,
For Max Shimba Ministries Org,
MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.
March 22, 2016

No comments:

KWANINI KRISMAS NI DISEMBA 25?

  TEREHE 25 DISEMBA IMETAJWA KWENYE BIBLIA KWANINI KRISMAS NI DISEMBA 25? Tuanze na kumsikiliza Yesu akiitumia aya inayo husisha tarehe 25 n...

TRENDING NOW